Shirika la Habari la Hawza - Semina ya kitaaluma na kiutamaduni yenye anuani “Kuelekea Amani Endelevu; Urithi wa Shahidi Ayatullah Imam Khamenei (ra)” ilifanyika katika Kituo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jijini Dar es Salaam.
Dios M. Kibamba, mhadhiri anayefahamika katika taaluma ya mahusiano ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Wizara ya Mambo ya Nje cha Tanzania, katika mada yake aliyoitoa kwa kuzingatia suala la sheria za kimataifa na amani endelevu, alikosoa utendaji wa mfumo wa kimataifa pamoja na taasisi za kimataifa.
Akirejea uzoefu wa Jumuiya ya Mataifa na maendeleo ya sheria za kimataifa, alisisitiza kwamba: Amani ya dunia itapatikana wakati kanuni ya usawa wa kisheria wa mataifa itakapotekelezwa kwa vitendo, na madola makubwa yasipoweza kutumia nguvu zao za kisiasa, kiuchumi au kijeshi kulazimisha matakwa yao kwa nchi nyingine.
Alisema: Uonevu, kujiona bora na kuwachukulia mataifa kwa viwango viwili tofauti ni miongoni mwa vikwazo vikubwa vya amani endelevu. Ili kufikia mfumo wenye haki zaidi, ni muhimu kufanyika marekebisho katika muundo na mifumo ya utaratibu wa kimataifa; utaratibu ambao ndani yake haki za mataifa zitaheshimiwa bila kujali kiwango cha nguvu na uwezo walionao.
Askofu Charles Howard, mwanachama wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani ya Tanzania, katika hotuba yake akirejea baadhi ya mafundisho na msisitizo wa Shahidi Ayatullah Imam Khamenei (ra), aliitaja amani na kuishi kwa pamoja kama miongoni mwa masharti muhimu zaidi ya maendeleo ya jamii.
Alisisitiza kwamba: Jamii za wanadamu haziwezi kufikia amani ya kweli bila kukubali tofauti zilizopo miongoni mwao na kuheshimiana.

Kwa mtazamo wa Howard, tofauti za maoni na tofauti zilizopo baina ya wanadamu ni jambo la kawaida, lakini kinachoweza kuisukuma jamii kuelekea kwenye mgogoro ni pale tofauti hizo zinapogeuzwa kuwa uadui na mgawanyiko.
Alisisitiza umuhimu wa kukubali tofauti, kuimarisha mazungumzo, kuwaheshimu wafuasi wa dini na tamaduni mbalimbali, pamoja na kukataa mifarakano na chuki. Aidha, aliitaja amani kuwa ni mchakato unaohitaji ushiriki wa matabaka yote ya jamii.
Sheikh Saleh Malbi, mhadhiri wa chuo kikuu nchini Tanzania, katika hotuba yake alizungumzia suala la kujiamini, kujitegemea na nafasi ya uongozi wa Mwenyezi Mungu katika uundaji wa jamii zinazojitegemea, akasema: Wakati jamii inapojengwa kwa kuzingatia maadili ya juu na utu wa mwanadamu, na wanadamu wote wanapokuwa na nafasi sawa mbele ya maadili ya Mwenyezi Mungu, mazingira ya kujenga na kujiamini kwa jamii hujitokeza.
Akirejea uzoefu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, aliieleza nchi hiyo kuwa ni mfano wa jamii ambayo imeweza kupiga hatua katika njia ya uhuru na kujitegemea, na kuweza kustahimili mashinikizo pamoja na utegemezi wa nje.
Kwa mujibu wa Malbi, kujiamini kwa mataifa ni miongoni mwa misingi muhimu zaidi ya kukabiliana na ukoloni na unyonyaji; kwa sababu taifa linaloamini katika uwezo wake hupata pia dhamira na uwezo unaohitajika wa kuamua mustakabali wake lenyewe.
Hujjatul-Isla'm Mahdi-Pour, katika hotuba yake hukuakirejea changamoto na mashinikizo makubwa ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekabiliana nayo katika miaka mbalimbali, alisisitiza kwamba: Kuvuka kwa Iran katika changamoto hizo hakukutokana tu na kuwa na vifaa na uwezo wa kijeshi, bali zaidi ya yote kulitokana na imani, dhamira na kujiamini wananchi katika uwezo wao wenyewe.
Akirejea uzoefu wa Iran, alisisitiza kwamba: Uhuru na maisha yenye heshima ya mataifa hayapatikani kwa nguvu za kijeshi pekee, bali yanahitaji haki, kuishi kwa pamoja, dhamira ya kukabiliana na dhuluma na ukosefu wa usawa, pamoja na kulinda heshima na uhuru wa mataifa.
Mahdi-Pour pia alisisitiza umuhimu wa mataifa kutegemea uwezo na rasilimali zao za ndani, pamoja na kudumisha umoja na dhamira ya pamoja wakati wa kukabiliana na mashinikizo kutoka nje.
Ima Nyerere, mwanaharakati wa kijamii na binti wa Julius Nyerere, katika hotuba yake akirejea uhusiano wa kirafiki na wa kihistoria baina ya Tanzania na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alisema: Tanzania kwa miaka mingi imekuwa na uhusiano wa kirafiki na Iran, na katika masuala kama vile haki na kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa, kuna mambo muhimu yanayozifananisha nchi hizi mbili.
Akirejea urithi wa fikra na siasa wa Julius Nyerere, alisisitiza kwamba: Misingi kama vile haki, uhuru, utu wa mwanadamu na kutetea haki za binadamu ilikuwa miongoni mwa misingi ya kuundwa Tanzania, na maadili haya bado yanaweza kuwa msingi wa ushirikiano na mshikamano baina ya mataifa.
Pembeni mwa semina hiyo, wageni na washiriki walitembelea maonesho maalumu ya Vita vya Tatu vya Kulazimishwa, yaliyokuwa yameandaliwa katika Kituo cha Utamaduni. Maonesho hayo yalikuwa na sehemu zilizohusu Minab, Lamerd na Shahidi Ayatullah Imam Khamenei (ra), na yaliwasilishwa kwa njia ya kazi mbalimbali na picha vipengele tofauti vya kiutamaduni na kijamii vya tukio hilo.
Aidha, waandishi wawili vijana ambao wameandika vitabu vinavyomhusu Shahidi Ayatullah Imam Khamenei (ra), walimkabidhi Hujjatul-Isla'am Mahdi-Pour, nakala za vitabu vyao.
Maoni yako